Jumapili 25 Oktoba 2026 - 12:25
Serikali ya Iraq Ipitie Upya Sera Zake za Kiuchumi na Iepuke Kujiingiza Vitani Upande wa Marekani

Hawza/ Ayatullah Sayyid Yasin al-Musawi ameitaka serikali ya Iraq kupitia upya sera zake za kisiasa na kiuchumi, huku akionya kuhusu madhara yanayoweza kutokana na kuiunga mkono Marekani katika mzozo unaoendelea dhidi ya Iran.

Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin al-Musawi, Imam wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad na mmoja wa walimu mashuhuri wa Hawza ya Najaf Ashraf, katika khutuba yake ya kisiasa ya Swala ya Ijumaa, iliyotolewa tarehe 23 Oktoba 2026 (1 Aban 1405 Hijria ya Shamsia), alisema kuwa maandamano yaliyofanyika nchini Ufaransa na katika baadhi ya nchi za Ulaya, na hatimaye nchini Marekani, kufuatia kupanda kwa bei na kuzorota hali ya uchumi, yanaonesha mabadiliko katika mizani ya kisiasa na kiuchumi duniani.

Aliongeza kuwa madhara ya vita dhidi ya Iran kwa sasa yanaathiri uchumi wa nchi za Magharibi pamoja na masoko ya nishati.

Alisema pia kuwa namna nchi za Magharibi zinavyokabiliana na maandamano inaonesha kuwepo kwa viwango viwili vya upimaji. Hii ni kwa sababu madola ya Magharibi, ambayo hukosoa namna serikali za nchi nyingine zinavyokabiliana na maandamano ya wananchi, yenyewe pia hutumia nguvu dhidi ya waandamanaji pale ambapo maandamano hayo yanapogusa maslahi yao ya ndani.

Alieleza kuwa misimamo hiyo inaonesha kuendelea kuwepo mantiki ya utawala wa kikoloni katika kusimamia mahusiano ya kimataifa; mantiki ambayo iko mbali na misingi ya kibinadamu ambayo nchi hizo hudai kuitetea.

Ayatullah al-Musawi, akigusia kupanda kwa bei ya mafuta na kuyumba masoko alisema kuwa; mabadiliko hayo yanahusiana na maendeleo ya matukio ya kivita katika eneo hili na katika Mlango-Bahari wa Hormuz. Alibainisha kuwa masoko ya dunia huzingatia zaidi hali halisi ya matukio yanayotokea katika uwanja wa mapambano kuliko kutegemea tu kauli za kisiasa.

Vilevile, alieleza kuwa maandamano nchini Marekani dhidi ya sera za Trump na vita dhidi ya Iran yanaonesha kuwa madhara ya kiuchumi ya mzozo huo yameanza kuikumba Marekani yenyewe. Hata hivyo, alisisitiza kuwa maandamano hayo hayamaanishi moja kwa moja kuwepo mshikamano wa kibinadamu na wananchi wa Iran.

Alisisitiza kuwa Iraq inapaswa kuzingatia maslahi yake ya kitaifa pamoja na hali halisi ya kijiografia na kisiasa wakati wa kuamua msimamo wake kuhusu mzozo huo. Alionya kuwa kuungana na Marekani dhidi ya Iran kunaweza kuiweka Iraq katika hatari ambazo haina uwezo wa kuzivumilia.

Ayatullah al-Musawi alisema kuwa; Iraq inakabiliwa na machaguo mawili ya msingi: Ima kujiingiza vitani upande wa mmoja wa wahusika katika mzozo huo, au kudumisha msimamo wake wa kutofungamana na upande wowote. Alisisitiza kuwa kuchukua msimamo wa uhasama dhidi ya Iran kwa kutegemea uungwaji mkono wa Marekani hakutokani na tathmini ya uhalisia wa mizani ya nguvu na maslahi.

Kuhusu manufaa ya kuitegemea Marekani ili iisaidie Iraq, Imam wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad alihoji faida ya matumaini hayo, huku akibainisha kuwa taarifa za vyombo vya habari zinaonesha kuondoka wanajeshi wa Marekani katika baadhi ya nchi za eneo hilo, zikiwemo Kuwait, Umoja wa Falme za Kiarabu na nchi nyingine.

Alisisitiza kuwa viongozi wa Iraq wanaohusika na kufanya maamuzi wanapaswa kuwasikiliza wananchi na kuzingatia maslahi yao kabla ya kuchukua maamuzi yanayoweza kuisababishia nchi hiyo makabiliano ya kijeshi au migogoro mikubwa zaidi ya kiuchumi.

Aidha, alionya dhidi ya kurudia uzoefu wa huko nyuma ambao, kutokana na tathmini isiyo sahihi ya mabadiliko ya kikanda na kimataifa, uliisababishia Iraq maafa makubwa.

Ayatullah al-Musawi pia aliyataka makundi ya kisiasa ya Iraq kubeba jukumu lao la kihistoria na kutoiendesha nchi kwa kutegemea misimamo ya kibinafsi au kauli za watu binafsi zinazodai kukubali kuwajibika wao wenyewe.

Alisema kuwa hatima ya nchi, uchumi wake na maisha ya wananchi haviwezi kusimamiwa kwa mantiki ya changamoto na ushindani wa kibinafsi, bali mambo hayo yanahitaji mfumo wa kitaasisi, uzoefu na mipango inayotegemea misingi ya kisayansi.

Katika sehemu ya kiuchumi, alisisitiza umuhimu wa kutofautisha kati ya “elimu ya uchumi” na “mkabala wa kiuchumi”. Alieleza kuwa usimamizi wa uchumi wa nchi hauishii katika kuwa na maarifa ya kitaaluma ya chuo kikuu au vyeti vya elimu, bali unahitaji uelewa wa mikabala mbalimbali ya kiuchumi inayoamua namna utajiri unavyogawanywa, rasilimali zinavyosimamiwa na uhusiano kati ya serikali na wananchi.

Sayyid al-Musawi, akirejelea kitabu Iqtisaduna (Uchumi Wetu), kilichoandikwa na Shahidi Ayatullah Sayyid Muhammad Baqir al-Sadr, aliwataka viongozi kutumia mitazamo ya kiuchumi iliyowasilishwa katika kitabu hicho ili kuelewa matatizo ya kiuchumi na kijamii.

Ayatullah al-Musawi alikosoa sera za kifedha ambazo zimesababisha kudhoofika uwezo wa kununua wa dinari ya Iraq na kucheleweshwa malipo ya mishahara. Alionya kuwa kupanda kwa bei na kushuka thamani ya mapato kumesababisha mishahara inayopokelewa kutotosheleza tena mahitaji ya familia kwa kipindi chote cha mwezi.

Vilevile, alifafanua kuwa kufungwa kwa vituo vya mipaka kati ya Iraq na Iran kumesababisha kupungua uingizaji wa baadhi ya bidhaa katika soko la Iraq, hali ambayo imeathiri bei za mazao ya kilimo na bidhaa nyingine muhimu za msingi.

Aliitaka serikali kufanya uchunguzi na tathmini ya kina kuhusu maamuzi yanayohusiana na vituo vya mipaka na biashara ya nje. Alisisitiza kuwa hatua za haraka zisizozingatia athari za moja kwa moja za maamuzi hayo kwa masoko na watumiaji hazipaswi kuchukuliwa.

Imam wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad alionya kuwa; kuendelea gharama kubwa za maisha, umaskini na kupungua kwa uwezo wa wananchi wa kununua bidhaa kunaweza kusababisha kuongezeka kwa maandamano ya wananchi.

Alisisitiza kuwa njaa na shinikizo la kimaisha ni miongoni mwa mambo hatari zaidi yanayotishia utulivu wa kijamii. Aliongeza kuwa; kutatua migogoro ya kiuchumi kunahitaji maamuzi yaliyofikiriwa kwa kina, sera zilizo wazi na kuwaeleza wananchi kwa uaminifu hali halisi iliyopo. Alionya kuwa hatua za haraka zisizotegemea utaalamu zinaweza kuongeza matatizo na mateso ya wananchi badala ya kuyapunguza.

Mwisho wa khutuba yake, Ayatullah al-Musawi alisisitiza kuwa ukosoaji wake unatokana na kujali maslahi ya Iraq na wananchi wake, wala si kwa sababu ya maslahi binafsi au kwa lengo la kuwatukana viongozi.

Alieleza matumaini yake kwamba Mwenyezi Mungu atawawezesha viongozi kufanya maamuzi sahihi na kuacha mbinu zisizo na busara, ili waweze kushughulikia kwa dhati migogoro ya kisiasa na kiuchumi, kulinda maslahi ya wananchi na, hasa, yale ya watu maskini na wenye kipato cha chini.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha